Jan 29, 2022 08:16 UTC
  • Waziri wa Sheria wa Libya anusurika kuuawa katika shambulio la watu wenye silaha

Vyombo vya habari vimetangaza kuwa Waziri wa Sheria wa Libya amenusurika kuuawa katika shambulio la watu wenye silaha lililotokea kwenye barabara ya As-Sawani katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.

Afisa mmoja wa usalama wa Libya amesema, waziri wa sheria Halima al-Busifi amenusurika kuuawa katika shambulio lililotokea katika barabara ya As-Sawani karibu na eneo la al-Aziziyah.

Afisa huyo amebainisha kuwa, gari moja la deraya lilisimamisha gari ya waziri huyo; na mtu mmoja aliyekuwa na silaha alishuka kwenye gari hilo la deraya na kuimiminia risasi gari ya waziri huyo lakini risasi hazikumpata.

Ameongeza kuwa, uchunguzi unaendelea kuwatambua waliohusika na jaribio hilo la mauaji.

Ofisi ya habari ya wizara ya sheria ya Libya imetoa taarifa na kuthibitisha kujiri kwa tukio hilo.

Mwezi uliopita, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya Abdulhamid Mohammed Al-Dabaiba alimkabidhi Halima al-Busifi jukumu la kushughulikia faili la mawaziri wa elimu na utamaduni ambao wamekamatwa na kuwekwa kizuizini.../

 

Tags