Jan 29, 2022 12:28 UTC
  • WFP: Asilimia 40 ya wakazi wa jimbo la Tigray Ethiopia wanajongewa na baa la njaa

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetangaza kuwa, takribani asilimia 40 ya wakazi wa jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Ripoti ya shirika hilo inaeleza kuwa, hali ya maafa katika jimbo la Tigray ilianza baada ya mashirika ya misaada kulazimika kupunguza kazi zao kutokana na ukosefu wa petroli na mahitaji mengine.

Wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya kibinadamu wanalazimika kutembea kwa miguu ili kwenda kutoa misaada kwa wakazi wanaohitajia misaada.

Shirika la WFP limesema kuwa, mapigano mapya pia yamesababisha njia za kupelekea misaada zipungue.

Tathmini iliyofanywa na Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, watu milioni 4.6 ambao ni asilimia 83 kwenye jimbo la Tigray hawana uhakika wa kupata chakula na watu wapatao milioni mbili kati ya hao wamo katika hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na baa la njaa.

Wakimbizi Tigray wakiwa katika foleni ya chakula cha msaada

 

Mkurugenzi wa WFP kanda ya Afrika Mashariki, Michael Dunford pia ametoa tahadhari kuhusu kuongezeka kwa njaa katika mikoa jirani ya Amhara na Afar, ambayo amesema imeathiriwa sana na mapigano katika miezi ya hivi karibuni.

Japokuwa mivutano na vita baina ya jeshi la serikali kuu na waasi Tigray vimekuwepo kwa muda mrefu, lakini mapigano mapya yaliyozuka kuanzia Novemba mwaka juzi (2020) ni makubwa kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni. Mapigano hayo yalianza baada ya viongozi wa jimbo la Tigray kufanya mambo kinyume na matakwa ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuhusiana na uchaguzi.