Feb 12, 2022 06:55 UTC
  • Rais wa Senegal alipongeza taifa la Iran kwa maadhimisho ya Siku ya Mapinduzi ya Kiislamu

Rais wa Senegal ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa serikali na taifa la Iran kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa 43 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Dakar, Mohammad Reza Dehshiri, ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, Rais Macky Sall wa Senegal amemtumia ujumbe Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutoa mkono wa baraka kwa serikali na taifa la Iran kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa 43 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika ujumbe wake huo, Rais Sall amesema kuwa, uhusiano wa nchi yake na Iran ni wa kuridhisha na kwamba Dakar iko tayari kuimarisha zaidi na zaidi uhusiano wake na Jamhuri ya Kislamu katika nyuga na sekta zote.

Rais Macky Sall wa Senegal

 

Sherehe za miaka 43 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran zilifikia kileleni jana Ijumaa tarehe 11 Februari 2022 na kuadhimishwa kwa ufanisi na hamasa kubwa katika kona zote za Iran na nje ya Iran.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalifikia kwenye ushindi siku ya Jumapili ya tarehe 11 Februari 1979 kwa uongozi wa mwanachuoni shujaa na mwanaharakati, Imam Khomeini MA. Kadiri miaka inavyopita ndivyo sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran zinavyozidi kunawiri na kufanyika kwa ufanisi na hamasa kubwa zaidi.

Tags