Feb 22, 2022 11:52 UTC
  • Mtaalamu wa UN awasili Sudan kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu baada ya mapinduzi ya jeshi

Mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa yuko nchini Sudan kuthibitisha madai ya wwa haki za binadamu baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo Oktoba mwaka jana ambayo yameitumbukiza nchi katika machafuko na kusababisha maandamano ya karibu kila siku dhidi ya utawala wa kijeshi.

Adama Dieng, mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Sudan, aliwasili katika mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum, siku ya Jumapili; mwezi mmoja baada ya mamlaka ya Sudan kuomba kuahirishwa kwa ziara yake.

Dieng alikuwa mshauri maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya halaiki na aliwahi kuwa mpelelezi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu nchini Rwanda.

Aliteuliwa mwezi Novemba mwaka jana kufuatilia hali ya haki za binadamu nchini Sudan baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 25.

Kazi ya Dieng ni kuthibitisha madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanyika Sudan wakati wa maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika tangu jeshi la nchi hiyo lilipotwaa madaraka ya nchi.

Mapinduzi hayo yamekwamisha harakati ya Wasudani ya kuelekea kwenye utawala wa kidemokrasia baada ya miongo mitatu ya ukandamizaji na kutengwa kimataifa chini ya uongozi wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar al-Bashir.

Sudan imekuwa katika mkwamo wa kisiasa tangu baada ya mapinduzi ya jeshi, huku wananchi wakiendelea kufanya maandamano ya kuwataka wanajeshi wakabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia na kurudi makambini.

Zaidi ya watu 80, wengi wao wakiwa vijana, wameuawa na wengine zaidi ya 2,600 kujeruhiwa katika maandamano hayo.

Wanawake wa Sudan wakiandamana kupinga mapinduzi ya jeshi

Vikosi vya usalama vya Sudan pia vimeshutumiwa kwa kutumia unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake wanaoshiriki katika maandamano hayo. 

Tags