Mar 21, 2022 06:42 UTC
  • Zaidi ya watu 6,000 wakimbia makazi yao nchini Gambia kutokana na mzozo wa Casamance, Senegal

Mamlaka ya Gambia imetangazai kwamba imehesabu zaidi ya watu 6,000 waliokimbia ghasia za wiki moja iliyopita kati ya jeshi na waasi wenye silaha katika eneo la Casamance kusini mwa nchi jirani ya Senegal.

Awali Jeshi la Senegal lilikuwa limetangaza kuwa limeanzisha operesheni dhidi ya wanamgambo waasi katika eneo la Casamance ambalo liko kusini mwa Gambia. 

Jeshi la Senegal limesema "lengo kuu la operesheni hiyo ni kubomoa kambi za kamanda wa waasi hao, Salif Sadio, zilizopo kando ya mpaka wa Gambia.

Shirika la Kitaifa la Kudhibiti Migogoro la Gambia limesema kwamba idadi ya watu wanaokimbia ghasia tangu Machi 13, imefikia watu 6,350, wakiwemo wakimbizi 4,508. 

Shirika hilo limeongeza kuwa, kutokana na hali ya eneo la Casamance la Senegal, eneo la Fonni-Kansala limekuwa kimbilio salama kwa wakimbizi na raia waliokimbia makazi yao  na kubainisha kuwa watu wa eneo hilo hawawezi tena kukaa katika nyumba zao kutokana na kukaribia mapigano kenye eneo hilo na athari mbaya za mzozo unaoendelea.

Eneo la Fonni-Kansala liko katika ardhi ya Gambia kwenye mpaka wa Casamance, karibu na eneo ambako mapigano yanafanyika kati ya jeshi la Senegal na wanamgambo wa Movement of Democratic Forces ambayo imekuwa ikipigania uhuru wa eneo hilo tangu 1982.

Mgogoro huo ulianza tena mwaka jana wakati Senegal ilipoanzisha mashambulizi ya kuwafukuza waasi hao. Rais wa Senegal, Macky Sall ametangaza suala la kurejesha amani huko Casamance kuwa ni kipaumbele kwa muhula wake wa pili.

Tags