Mar 28, 2022 11:07 UTC
  • Wananchi wa Burkina Faso waandamana kupinga uhusiano wa kijeshi na Ufaransa

Wananchi wa Burkina Faso wamefanya maandamano ya kushinikiza kuhitimishwa uhusiano na ushirikiano wa kijeshi baina ya nchi yao na Ufaransa.

Maandamano hayo yaliitishwa na muungano wa vyama vya kiraia nchini humo ambao umeitaka serikali mpya ya mpito nchini humo iliyoanza kazi mapema mwezi huu kusimamisha ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi na Ufaransa.

Muungano huo unaojulikana kama Unification Bureau sambamba na kutaka kukatwa uhusiano wa kijeshi na nchi hiyo ya Ulaya, lakini pia umesisitiza kuwa, unafadhilisha ushirikiano wa nchi yao na Russia katika vita dhidi ya magenge ya kigaidi.

Nchi nyingi za Kiafrika katika miezi ya hivi karibuni zimetangaza kukata au kupunguza uhusiano na ushirikiano wao hususan wa kijeshi na kiulinzi na Ufaransa.

Mwezi uliopita, mamia ya waandamanaji waliitikia mwito wa vyama vya upinzani wa kufanya maandamano dhidi ya wanajeshi wa mkoloni Mfaransa pamoja na utawala wa kijeshi nchini Chad.

Siku chache kabla ya hapo, serikali ya mpito ya Mali iliitaka Ufaransa kuwaondoa bila kuchelewa askari wake wa operesheni Barkhane na Takuba nchini Mali. Mivutano baina ya Ufaransa na Mali imeongezeka mno katika miezi ya hivi karibuni  hasa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana (2021).

Wananchi za nchi tatu za Mali, Burkina Faso na Niger wanayalaumu madola ya Ulaya hasa Ufaransa kwa kuchochea machafuko katika maeneo hayo na kuyapa misaada ya kila namna magenge ya kigaidi. 

Tags