Mar 30, 2022 03:00 UTC
  • Mkuu wa Benki ya Maendeleo Afrika: Vita vya Ukraine vinaweza kusababisha mgogoro wa chakula Afrika

Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) ambayo ni mkopeshaji mkubwa barani humo anafanya kila awezalo kuzuia bara la Afrika lisikabiliwa na mgogoro wa chakula kutokana na athari mbaya za vita vya Rusia na Ukraine.

Huku vita kati ya Russia na Ukraine vikiingia katika mwezi wake wa pili, bei ya gesi asilia, ngano na mbolea imepanda sana duniani. Russia na Ukraine zinazalisha zaidi ya robo ya ngano inayouzwa nje duniani; na bara la Afrika linazitegemea pakubwa nchi mbili hizo.

Nchi za Afrika zinanunua asilimia 90 ya ngano yenye thamani ya dola bilioni 4 kutoka Russia na linafanya biashara na Ukraine ya karibu dola bilioni 4.5.  

 Mkuu wa Benki ya Maendeleo Afrika, Akinwumi Adesina, amesema kuwa, theluthi moja ya nafaka zinazotumiwa Afrika Mashariki inatoka katika nchi mbili hizo; huku Misri ikiwa imeathirika pakubwa. Hali kama hii inashuhudiwa pia huko Algeria, Morocco na Somalia na katika nchi nyingine kadhaa. Amesema iwapo hali hii haitadhibitiwa haraka iwezekanavyo, bara la Afrika litayumba.

Akinwumi Adesina

Amesema vita vya Russia na Ukraine vitaathiri uchumi wa Afrika kwa njia kuu kadhaa na tayari vimesababisha mtikisiko katika masoko la fedha na kupandisha juu viwango vya riba.

Mkuu wa Benki ya Maendeleo Afrika amesema, pengine muhimu zaidi ni kwamba, bei za bidhaa zinaongezeka, ikiwa ni pamoja na ile ya ngano ambayo imepanda kwa asilimia 64 duniani.

Amesema: "Vita hivyo vimeibua mfumuko wa bei barani Afrika, na iwapo havitadhibitiwa vitasababisha mgogoro wa chakula barani Afrika,"

Tags