Apr 03, 2022 08:16 UTC
  • 20 wauawa katika shambulio la kigaidi dhidi wa mgodi wa dhahabu Burkina Faso

Watu wasipoungua 20 wameuawa katika shambulio la watu wenye silaha kwenye mgodi mmoja wa dhahabu kaskazini mwa Burkina Faso.

Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, watu hao waliuawa baada ya magaidi waliokuwa juu ya pikipiki kuwamiminia risasi katika mgodi mdogo wa Kougdiguin katika kijiji cha Barga kilichoko mjini Bouroum, mkoa wa Namentenga.

Hakuna taarifa zaidi iliyotolewa kuhusiana na shambulio hilo, wala kundi la kigaidi lililohusina nalo.

Hata hivyo hujuma hiyo inajiri siku chache baada ya watu 11 kuuawa katika shambulio jingine la watu wenye silaha kwenye mgodi mmoja wa dhahabu katika eneo la Baliata kaskazini mwa nchi.

Mgodi wa dhahabu Burkinabe

Watu zaidi ya 80 wameuawa katika mashambulio dhidi ya migodi ya dhahabu nchini Burkina Faso katika wiki za hivi karibuni.

Burkina Faso ina kasi kubwa ya uzalishaji wa madini ya dhahabu barani Afrika na kwa sasa inashika nafasi ya tano katika uzalisha wa madini hayo. Karibu watu milioni 1.5 wanafanya kazi katika sekta ya madini ya dhahabu nchini Burkina Faso na mapato ya madini hayo yenye thamani kubwa na yanayopendwa sana duniani kwa mwaka 2019 ilitangazwa kuwa ni karibu dola bilioni 2. 

Tags