Apr 04, 2022 11:23 UTC
  • Magaidi 7 wa al-Shabaab waangamizwa na jeshi la Somalia eneo la Mudug

Kikosi maalumu cha Danab cha Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) kimefanikiwa kuwaangamiza wanachama saba wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katikati ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Odowa Yusuf Rage, Kamanda wa SNA amesema magaidi hao waliangamizwa jana Jumapili katika operesheni ya kikosi cha Danab karibu na mji wa Wisil, wilaya ya Hobyo, katika eneo la Mudug la katikati ya nchi.

Amesema wamefanikiwa kuwatia mbaroni wanachama wawili wa genge hilo la kigaidi, waliyojeruhiwa vibaya kwenye operesheni hiyo.

Rage amesema jeshi la Somalia limefanikiwa pia kutwaa silaha zilizokuwa zinatumiwa na magaidi hao, yakiwemo mabomu manne ya kuelekezwa kutoka mbali (IED), bunduki nne aina ya AK47 na gari walilokuwa wakilitumia.

Wanajeshi wa Somalia kazini

Kamanda huyo wa ngazi ya juu wa Jeshi la Taifa la Somalia amesema wataendeleza operesheni za kupambana na magaidi hao wakufurishaji katika jimbo la Galmudug, ambalo lilikamilisha uchaguzi wa Bunge wiki mbili zilizopita.

Haya yanajiri siku chache baada ya Kikosi cha mpito cha Umoja wa Afrika (ATMIS) kuanza kazi zake rasmi Ijumaa iliyopita, baada ya kupanguliwa Kikosi cha Kijeshi cha Umoja wa Afrika nchini humo (AMISOM).

ATMIS inatazamiwa kumaliza shughuli zake kufikia mwaka 2024, na karibuni itaanza mchakato wa kukabidhi jukumu la usalama wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kwa Jeshi la Taifa la Somalia.

 

Tags