Apr 07, 2022 11:16 UTC
  • EU yaeleza wasiwasi wake kuhusu kambi za mateso nchini Uganda

Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Ulaya katika Masuala ya Haki za Binadamu ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuteswa wafungwa na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu nchini Uganda.

Eamon Gilmore ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuteswa kwa wafungwa nchini Uganda wakati wa mazungumzo yake na Rais Yoweri Museveni na ametoa wito wa kukomeshwa ukandamizaji huo na kuwajibishwa wale wote waliohusika na uhalifu huo.

Gilmore amesema Rais wa Uganda ameahidi kwamba atashughulikia faili hilo.

Ziara ya afisa huyo wa Umoja wa Ulaya nchini Uganda imefanyika wiki mbili baada ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kutoa ripoti iliyoashiria mateso yanayofanyika katika jela zisizo za kisheria nchini Uganda na kuitaka serikali kufunga vituo na vizuizi visivyo halali vinavyotumiwa na vyombo vya usalama ili kukandamiza wapinzani.

Bobi Wine

 Human Rights Watch imeashiria vifo vya watu 51, wakiwemo wafungwa 34 wa zamani na mashahidi wa utekaji nyara, ambao walikuwa wahanga wa unyanyasaji wa polisi, jeshi na idara za upelelezi kati ya Aprili 2019 na Novemba 2021.

Wapinzani walikandamizwa vikali wakati wa uchaguzi wa Januari 2021, ambao kambi ya upinzani inadai ulikuwa wa kimaonyesho tu. Rais Yoweri Museveni ambaye amekuwa madarakani tangu 1986, alichaguliwa tena  kuongzoa nchi hiyo katika uchaguzi huo.

Ripoti ya Human Rights Watch imekusanya simulizi za wafuasi wa vyama vya upinzani na waandamanaji wa kawaida kuhusu visa cha kukamatwa kwao..

Tags