Apr 08, 2022 03:24 UTC
  • Ibrahim Al-Ghandour
    Ibrahim Al-Ghandour

Mahakama ya Sudan imemwachia huru Mkuu wa Chama cha National Congress Party (chama tawala zamani), Ibrahim Al-Ghandour na wengine 12 waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuhujumu utaratibu wa kikatiba na kufadhili ugaidi. Uamuzi wa mahakama hiyo umetajwa kuwa wa mwisho usioweza kukatiwa rufaa.

Chama cha National Congress Party kimetangaza katika taarifa yake kwamba, Mahakama ya Sudani imetangaza uamuzi wa kuwaondoa hatiani washtakiwa wote, ambao ni Ibrahim Ghandour na viongozi wengine 12  wa chama hicho baada ya kesi iliyochukua takriban miezi 22.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, shahidi mkuu wa mashtaka amekanusha maelezo yote yaliyokuwa yamewasilishwa mahakamani na kusema kuwa si sahihi na kwamba washtakiwa wote hawana hatia.

Ghandour na wenzake 12 walishutumiwa kwa kuhujumu utaratibu wa kikatiba, kufadhili ugaidi, kujaribu kumuua Waziri Mkuu wa zamani wa Sudan, Abdullah Hamdok, na kulipua kituo cha mafuta cha Berri.

Itakumbukwa kuwa, mwezi Machi 2020, Waziri Mkuu wa zamani wa Sudan, Abdullah Hamdok alikumbwa na jaribio la kumuua akiwa njiani kuelekea makao makuu ya Waziri Mkuu, lakini alinusurika jaribio hilo.

Abdullah Hamdok

Chama cha National Congress Party kiliondolewa madarakani nchini Sudan mnamo Aprili 11, 2019, baada ya jeshi la Sudan kumpindua rais wa wakati huo, Omar al-Bashir aliyeitawala nchi kwa kipindi cha miongo 3. Hatua hiyo ya jeshi ilifuatia maandamano ya wananchi waliokuwa wakipinga hali mbaya ya kiuchumi nchini humo.

Tangu wakati huo, mamlaka ya Sudan imekamata makumi ya vinara wa utawala wa zamani kwa tuhuma za kujaribu kupindua serikali.

Tags