Apr 08, 2022 13:06 UTC
  • Sensa Tanzania: Rais Samia atangaza tarehe ya kuhesabiwa Watanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniza, Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi nembo ya sensa na kutangaza kuwa siku ya sensa ya watu na makazi nchini humo itakuwa Jumanne Agosti 23, mwaka huu 2022.

Rais Samia amefanya uzinduzi wa nembo na kutangaza siku hiyo ya sensa leo Ijumaa Aprili 8, 2022 katika hoteli moja mjini Unguja, visiwani Zanzibar. Amesema shughuli ya kuhesabu watu inaisaidia Serikali kupanga vyema mipango yake ya maendeleo.

Amenukuliwa na gazeti la Mwananchi akieleza kuwa, "Hili sio jambo geni, kwa hiyo ni muhimu na tujitahidi kukamilisha mipango hii kwa manufaa ya Taifa letu." 

Rais wa Tanzania ameagiza nembo hiyo itumike kwa shughuli zote za kiserikali na taasisi binafsi ili kuhamasisha wananchi waweze kutambua umuhimu wa kuhesabiwa.

Rais Samia amebainisha kuwa, "Kwa taasisi za Serikali nembo hii iwekwe kwenye machapisho na mitandao ya kijamii lakini kwa upande wa taasisi binafsi zinaweza kuwekwa hata kwenye vifungashio au risiti na tiketi, kikubwa kila sehemu tuone hiyo nembo." 

Bendera ya Tanzania

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema siku ya sensa imepangwa kwa kuzingatia maombi ya viongozi wa dini isiwe siku ya ibada.

Majaliwa amesema mpaka sasa maandalizi ya shughuli hiyo ya sensa yamefikia asilimia 79 na kwamba kazi hiyo inaendelea kuratibiwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya Serikali zote mbili; Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibari.

Tags