Apr 09, 2022 12:16 UTC
  • UN: Somalia iko hatarini kukumbwa na njaa

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa Somalia kwa sasa iko katika hatari ya kukumbwa na njaa kutokana na ukame, bei ya juu ya vyakula na ukosefu wa misaada ya kibinadamu.

Stéphane Dujarric amesema, inatazamiwa kuwa maeneo sita ya Somalia yatakabiliwa na hatari ya njaa na ukame kuanzia sasa hadi mwezi Juni iwapo kutaendelea kushuhudiwa uhaba wa mvua.

Dujarric Ameongeza kuwa: "Ukame unazidi kuongezeka kote nchini Somalia na inakadiriwa kuwa watu milioni 4.9, wakiwemo wakimbizi wa ndani 719,000, wataathirika na janga hilo."

Msemaji wa Antonio Guterres pia alisema kuwa zaidi ya asilimia 80 ya vyanzo vya maji vinakauka na kwamba viwango vya maji vya mito Shabelle na Juba vimefikia chini kabisa.

Stéphane Dujarric

Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa, makadirio yanaonyesha kuwa takriban watu milioni 3.5 kwa sasa hawana maji ya kutosha nchini Somalia.

Dujarric pia amesema kuwa zaidi ya watoto milioni 1.4 walio chini ya umri wa miaka mitano wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo mkali mwaka huu katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Hapo awali Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilitangaza kuwa ukame umesababisha takriban watu milioni 13 katika eneo la Pembe ya Afrika kukumbwa na njaa.

Tags