Apr 12, 2022 10:26 UTC
  • Libya yakataa kucheza na Israel mchezo wa vitara huko Imarati

Timu ya taifa ya mchezo wa kushindana kwa vitara (fencing) ya Libya imekataa kucheza na utawala haramu wa Israel katika mashindano ya ubingwa wa mchezo huo katika Umoja wa Falme za Kiarabu, ili kuonesha mshikamano wao kwa wananchi wa Palestina.

Timu hiyo ilijiondoa kwenye fainali ya mashindano hayo mjini Dubai siku ya Jumapili, licha ya kufanya vizuri katika mapambano yake yote kwenye mashindano hayo ya dunia yanayojulikana kama World Fencing Championships.

Tovuti ya Libya Observer imeripoti habari hiyo na kueleza kuwa: Timu ya taifa ilipaswa kukutana na Israel kwa mujibu wa droo iliyochezeshwa. Hata hivyo wachezaji na benchi la ufundi waliamua kujiondoa kwenye mashindano haya, kukwepa kukutana na hasimu Israel.

Timu hiyo ya Libya ya mchezo wa vitara ambayo ipo katika nafasi ya pili barani Afrika na 19 duniani katika orodha ya mchezo huo aidha imekataa kucheza na Wazayuni kupinga hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo pandikizi.

Wanamichezo kadhaa wa nchi za Kiarabu wamekataa kuwa sehemu ya sera za kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel ambao unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina, kwa kususia kucheza na Wazayuni.

Mapema mwaka huu, mchezaji maarufu wa mchezo wa tenisi kutoka Kuwait, Muhammad Al Awadi alijiondoa katika Mashindano ya J4 Dubai ambayo yalifanyika huko Imarati kuanzia Januari 17 hadi 22, ili asikutane na Mzayuni.

Agosti mwaka jana pia, mwanajudo wa Lebanon, Abdullah Miniato alitangaza kujiondoa katika mashindano ya kimataifa ya mchezo wa Mixed Martial Arts (MMA) huko mjini Sophia, Bulgaria, na kwa utaratibu huo akawa judoka wa tatu kukwepa kuvaana na hasimu kutoka Israel katika mashindano ya Olimpiki ya Tokyo, baada ya wanajudo wengine wawili kutoka Algeria na Sudan kukataa kupambana na washindani wao za Kizayuni.

 

 

Tags