Apr 13, 2022 07:48 UTC
  • UN: Tunatumai uthabiti na usalama utarejea nchini Somalia karibuni

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ana matumaini ya kurejeshwa uthabiti, amani na usalama nchini Somalia haraka iwezekanavyo.

António Guterres alieleza matumaini hayo katika mazungumzo yake ya simu na Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi Mohamed ‘Farmajo’ na kusisitiza kuwa, UN imesimama na nchi hiyo ya Pembe ya Afrika mkabala wa ongezeko la mashambulizi ya kundi la kigaidi la al-Shabaab na ukame unaolisumbua taifa hilo.

Kadhalika Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha hatua ya kupanguliwa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) na kuundwa kikosi kipya cha mpito cha ATMIS.

Askari wa AU nchini Somalia

Guterres amesema anatumai kuwa Somalia karibuni hivi itaweza kujidhaminia usalama wake. Kikosi hicho cha mpito cha Umoja wa Afrika (ATMIS) kilianza kazi Aprili Mosi, siku moja baada ya AMISOM kumaliza jukumu lake la kuidhaminia usalama Somalia na kupambana na magenge ya kigaidi kwa miaka 15. ATMIS inatazamiwa kumaliza shughuli zake mwaka 2024.

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 na katika miaka ya hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wakufurishaji wa Al Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.

 

Tags