Apr 13, 2022 07:58 UTC
  • Viongozi wa Waislamu Uganda wazika tofauti zao, wapania kuunda taasisi moja

Viongozi wa makundi na mashirika ya Kiislamu nchini Uganda wametangaza kuungana na kusuluhisha tofauti zao, sanjari na kusaini makubaliano ya kuunda taasisi moja itakayowaleta pamoja na kuwaunganisha.

Viongozi hao wa Kiislamu nchini Uganda wakiongozwa na Mufti Mkuu wa nchi hiyo, Sheikh Shaban Ramadhan Mubajje jana Jumanne walimtembelea Rais Yoweri Museveni katika Ikulu ya Entebbe, na kumtaarifu kuhusu kuungana kwa jumuiya na taasisi za Kiislamu nchini humo na kuwa kitu kimoja.

Sheikh Mubajje amesema walisaini 'Muafaka wa Umoja' baina ya Baraza Kuu la Waislamu Uganda (UMSC), na makundi hasimu ya Kibuli na Nakasero, katika Msikiti wa Jamia wa Gaddafi jijini Kampala, kabla ya kwenda kukutana na Museveni.

Rais Museveni kwa upande wake amewapongeza viongozi hao wa Kiislamu kwa kuamua kuzika tofauti zao na kufanya kazi bega kwa bega akisisitiza kuwa, serikali yake kwa muda mrefu sana imekuwa ikitilia mkazo suala la umoja na mshikamano miongoni mwa watu wa dini, kabila na madhehebu tofauti.

Waislamu wa Uganda wakitekeleza ibada ya Swala

Amesema: Katika miaka minane ya kupambana na (Iddi) Amin, nilisaidiwa sana na (viongozi wa Waislamu) kama Abbas Kibazo wa Kibuli na Zubair Bakali miongoni mwa wengine. Kwa hivyo hatua ya kuungana na makundi yote yakiwemo wa Waislamu yalitusaidia kupata ushindi, kwani umoja ni nguvu.

Viongozi wengine wa Waislamu wa Uganda waliokuwemo kwenye ujumbe uliomtembelea Rais Museveni katika Ikulu ya Entebbe ni pamoja na Sheikh Obeid Kamulegeya, Sheikh Muhammed Yunusu Kamoga, Sheikh Muhamood Kibaate, Sheikh Kasule Ndirangwa na Sheikh Hamid Umar Kateregga.

Tags