Apr 14, 2022 07:13 UTC
  • Afrika Kusini yaongeza muda wa kuhudumu wanajeshi wake huko Msumbiji

Mkuu wa jeshi la Afrika Kusini ametahadharisha kuwa magaidi waliopo Msumbiji lazima washughulikiwe kabla ya tatizo hilo kuenea mbali zaidi.

Rudzani Maphwanya ameeleza hayo akizungumza huko Pretoria kufuatia makubaliano yaliyofikiwa mapema wiki hii kwa ajili ya kupanua kikosi cha pamoja cha jeshi kwa ajili ya kupambana na magaidi nchini Msumbiji. 

Rudzani Maphwanya, Mkuu wa Jeshi la Afrika Kusini 

Wanajeshi wa Afrika Kusini ni sehemu ya kikosi cha wanajeshi kutoka nchi 16 za Jumuiya ya SADC kwa jina la SAMIM chenye lengo la kuisaidia Msumbiji katika vita dhidi ya magaidi katika mkoa wa Cabo Delgado, Kaskazini mwa nchi hiyo. Mapambano dhidi ya magaidi nchini Msumbiji yalianza mwezi Julai mwaka jana. 

Nchi nyingine zinazochangia katika kikosi hicho ni Angola, Botswana, Congo, Lesotho, Malawi, Tanzania na Zambia. Wakati huo huo Rwanda imetuma wanajeshi nchini humo kama sehemu ya makubaliano ya pande mbili na serikali ya Msumbiji. 

Mkutano huo wa kilele uliofanyika chini ya uwenyekiti wa Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ulikuwa pia fursa ya kutathmini wanajeshi wa karibuni ndani ya kikosi hicho cha SAMIM.  

Wanajeshi wasiopungua 600 kutoka jeshi la ulinzi wa taifa la Afrika Kusini wamekuwepo katika jimbo la Cabo Delgado kati ya Oktoba mwaka jana na Januari mwaka huu kama sehemu ya "Oparesheni ya Buffalo."

Tags