Apr 15, 2022 04:00 UTC
  • UN: Watoto 350,000 wa Somalia katika hatari ya kufa njaa

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa, watoto 350,000 wapo katika nchi ya kupoteza maisha kutokana na baa la njaa linaloisakama Somalia.

Adam Abdelmoula, ofisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) amesema: Tunavyozungumza sasa, watoto milioni 1.4 wa Kisomali wenye chini ya miaka mitano wanasumbuliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu, na iwapo hatua za dharura hazituchukuliwa, 350,000 miongoni mwao wataaga dunia kabla ya msimu wa joto mwaka huu.

Amesema, "Ninatoa mwito kwa wote wanaoweza kuchangia, wakiwemo Wasomalia walioko ughaibuni, wafanyabiashara, wafadhali wa ada na wasio wa ada, kila mtu kuchukua hatua sasa hivi."

Ukame unaoisumbua Somalia sasa hivi haujawahi kushuhudiwa kwa miaka 70

Umoja wa Mataifa umetoa ombi la kutolewa misaada ya haraka ya kuweza kuwaokoa wananchi wa Somalia kutokana na ukame kuhatarisha vibaya maisha ya asilimia 40 ya wananchi wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO pamoja na mashirika ya OCHA, UNICEF na WFP ambayo yote yanafanya kazi chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa yalisema hivi karibuni kuwa, watu milioni sita wanakabiliwa na uhaba wa chakula nchini Somalia, na misaada ya haraka mno inahitajika ili kuokoa maisha yao. 

Tags