Apr 16, 2022 02:25 UTC
  • Benki ya Dunia: Idadi ya maskini nchini Nigeria kupindukia milioni 95

Benki ya Dunia imetahadharisha kuwa, idadi ya watu wanaosumbuliwa na umaskini na ukata wa kupindukia nchini Nigeria itaongezeka na kufikia watu milioni 95.1 mwaka huu 2022.

Taasisi hiyo ya kimataifa ya fedha imesema sababu kuu ya ongezeko hilo la watu maskini nchini Nigeria ni kudororo kwa uchumi wa taifa hilo la Afrika Magharibi lenye utajiri wa mafuta.

Wakala wa Jobberman, ambayo ni taasisi kubwa zaidi ya masuala ya ajira katika eneo la Afrika Magharibi imesema katika ripoti yake kuwa, asilimia 47 ya wanachuo waliofuzu kwa kozi mbalimbali katika Vyuo Vikuu vya Nigeria hawana kazi, na kiwango cha umaskini kinaongezeka kwa kiasi cha kutisha.

Kwa mujibu wa Jobberman, janga la ugonjwa wa COVID-19, utegemezi wa bidhaa na vyombo kutoka nje ya nchi, na kupoteza thamani sarafu ya Naira ni miongoni mwa mambo yaliyochangia watu wengi kupoteza au kukosa nafasi za ajira. 

Janga la Corona pekee limepelekea Wanigeria wengine milioni 5 kutumbukia katika umaskini wa kupindukia mwaka huu.

Hii ni katika hali ambayo, huko nyuma, ripoti ya Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ilionya kuwa, watu milioni 50 katika nchi za Afrika watatumbukia katika lindi la umaskini wa kupindukia kutokana na makali ya janga la Corona.

Kwa mujibu wa chunguzi za hivi karibuni na utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia, maambukizi ya Corona yamesababisha watu zaidi ya nusu bilioni kuwa maskini duniani.

Tags