Apr 17, 2022 08:07 UTC
  • AU kumtimua mkuu wa kikosi chake cha mpito nchini Somalia

Mkuu wa kikosi kipya cha kijeshi cha mpito (ATMIS) kilichochukuwa nafasi ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) yupo katika mashinikizo ya kutakiwa ajiuzulu baada ya kushtadi msuguano wa kidiplomasia kati yake na serikali ya Mogadishu.

Duru za habari zimeliambia gazeti la The East African kuwa, Balozi Francisco Madeira anashinikizwa ajiuzulu ili isionekane kuwa amefukuzwa kazi na kikosi hicho cha mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia.

Tayari serikali ya federali ya Somalia kupitia Waziri wa Usalama Abdullahi Noor imeagiza kufutwa kibali cha kumruhusu mwanadiplomasia huyo raia wa Msumbiji kuingia katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Baadhi ya maafisa wa Somalia wamekuwa wakimtuhumu Mkuu huyo wa kikosi kipya cha kijeshi cha mpito cha ATMIS kuwa anaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Balozi Madeira anakabiliwa na mashinikizo ya kujiuzulu katika hali ambayo, amekuwa akiungwa mkono na Rais anayeondoka wa Somalia, Mohammed Abdullah "Farmajo" na vilevile Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, Mousa Faki Mahamat. 

Wanajeshi wa AU nchini Somalia

Hata hivyo wamekuwa wakilumbana na Waziri Mkuu wa Somalia, Mohamed Hussein Roble, ambaye siku chache zilizopita aliagiza apokonywe leseni zake za kazi, na asiruhusiwe kutumia lango na ukumbi wa Watu Mashuhuri (VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Adde.

Kikosi cha ATMIS kilichoanza kazi mapema mwezi huu kikirithi mikoba ya AMISOM iliyohudumu kwa karibu miaka 15, kinatazamiwa kumaliza shughuli zake mwaka 2024.

 

Tags