Apr 18, 2022 13:05 UTC
  • Wakimbizi wa Kisomali wakabiliwa na hali ngumu katika mfungo wa Ramadhani

Zaidi ya wakimbizi milioni moja wa Kisomali hususan wale wanaoishi katika kambi za nje ya mji mkuu, Mogadishu, wanakabiliwa na hali ngumu katika mfungo huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Ukame umeziathiri jamii za wafugaji na wakulima katika maeneo ya Kusini na Kusini Mashariki mwa Ethiopia, Kusini Mashariki na Kaskazini mwa Kenya na Kusini Kati huko Somalia; huku kiwango cha utapiamlo katika maeneo hayo kikiongezeka pakubwa. 

Tovuti la al Arabi Jadid imeripoti kuwa, wakimbizi hao wa Kisomali wanaishi katika mazingira magumu sana na hawana uwezo wa kumudu mahitaji yote ya lazima katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani. Wakimbizi hao wanaoishi katika kambi zilizo nje ya mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, hawana fedha huku bei za bidhaa mbalimbali ikiwemo chakula, zikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 wakati huu wa mwezi wa Ramadhani. Kupanda huko kwa gharama za maisha wakati huu kumewafanya raia hao waishi katika hali ngumu sana. 

Huko nyuma pia raia hao wa Kisomali walikabiliwa na hali ngumu katika msimu wa kiangazi; kwa kuishi katika joto kali mchana kutwa na kukosa huduma ya umeme. Kilowati moja ya umeme inauzwa karibu nusu dola.    

Stephane Dujaric msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hivi karibuni alitahadharisha kuwa, Somalia inakabiliwa na hatari ya njaa ikiwa ni matokeo ya ukame, kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali za vyakula na kutotumwa misaada ya kibinadamu nchini humo. 

Tags