Apr 20, 2022 02:48 UTC
  • Eritrea yakosoa mpango 'haramu' wa kuwahamishia Rwanda wakimbizi wa Uingereza

Serikali ya Eritrea imekosoa makubaliano ya kuwahamishia Rwanda wakimbizi kutoka Uingereza ikisisitiza kuwa, mpango huo haukubaliki, unashtua na unapaswa kupingwa na kulaaniwa vikali.

Katika taarifa, Wizara ya Habari ya Eritrea imesema taifa hilo la Pembe ya Afrika linayatazama mapatano hayo ya London an Kigali kama mpango haramu wa kufanya magendo ya binadamu.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, mpango huo wa kuwahamishia kwa nguvu wakimbizi na watafuta hifadhi nchini Rwanda kutoka Uingereza unalenga kuficha sababu halisi na mambo yanayoshadidisha masuala ya ukimbizi na magendo ya wanadamu duniani.

Wizara ya Habari ya Eritrea imebainisha kuwa, baadhi ya serikali zinafuatilia sera za kupunguza idadi ya watu katika nchi zao mkabala wa nchi nyingine, kwa malengo fiche ya kisiasa.

Wakimbizi

Kabla ya hapo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilisema hivi karibuni katika taarifa yake kwamba linapinga vikali makubaliano hayo ya Uingereza na Rwanda, ambayo yalichapishwa hivi karibuni kwa ajili ya kuwahamishia Rwanda wahamiaji wanaotafuta hifadhi nchini Uingereza.

Makubaliano hayo yenye utata baina ya nchi mbili za Rwanda na Uingereza yamelalamikiwa vikali na nchi mbalimbali duniani ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na pia taasisi zaidi ya 160 za kutoa misaada na kutetea haki za binadamu. 

Uingereza ilifikia makubaliano hayo na serikali ya Kigali baada ya kushindwa kufikia mapatano kama hayo na nchi za Ghana na Albania. Serikali ya Rwanda itapewa dola milioni 158 na serikali ya Uingereza kwa kukubali kupokea wakimbizi hao.

Tags