Apr 22, 2022 13:10 UTC
  • Rais wa zamani wa Kenya, Mwai Kibaki afariki dunia akiwa na miaka 90

Rais mstaafu wa Kenya, Emilio Mwai Kibaki amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90. Mzee Kibaki aliyezaliwa Novemba 15, 1931, aliliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kati ya mwaka 2002 na 2013.

Hayo yametangazwa leo Ijumaa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika hotuba yake kwa taifa. Kibaki alikuwa Rais wa Tatu tangu Kenya ijinyakulie uhuru mwaka 1963.

Rais Kenyatta amemtaja Kibaki kama kiongozi aliyekuwa katika mstari wa mbele kuimarisha uchumi wa Kenya.

Amesema, “Mwai Kibaki atakumbukwa kwa weledi wake na bidii yake kazini. Kwa mujibu wa mamlaka yangu kama Rais wa Kenya, ninaamuru kwamba bendera ya Kenya itapeperushwa nusu mlingoti nchini na katika balozi zote za Kenya katika mataifa ya kigeni kuanzia leo Ijumaa hadi Rais Mstaafu Kibaki atakapozikwa.” 

Rais Kenyatta

Kibaki aliingia Ikulu kupitia kwa tiketi ya National Rainbow Coalition (NARC) na akaapishwa Desemba 30, 2002, kutumikia taifa kama Rais wa Tatu Jamhuri ya Kenya. Alihudumu kama kiongozi wa Taifa na Serikali hadi Aprili 9, 2013, alipokabidhi mamlaka kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Rais Kenyatta amesema japo taifa linaomboleza, lakini pia ni muhimu kukumbuka wakati ambapo Kibaki alitumikia taifa pamoja na wakati mzuri aliofurahia na mkewe Mama Lucy Kibaki ambaye naye alitangulia mbele ya haki 26 April 26, 2016, South Kensington, London, Uingereza.

 

Tags