Apr 23, 2022 02:49 UTC
  • Morocco yaendeleza siasa za kindumilakuwili kuhusu wananchi wa Palestina

Baada ya serikali ya kifalme ya Morocco kufanya usaliti dhidi ya kadhia ya Palestina ambayo ndiyo muhimu zaidi kwa Umma wa Kiislamu, na baada ya Rabbat kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala pandikizi wa Kizayuni, hivi sasa nchi hiyo inajifanya kuguswa na jinai za Israel.

Serikali ya Morocco imemwita balozi wa utawala wa Kizayuni mjini Rabbat kumuelezea wasiwasi wake kutokana na wanajeshi makatili wa Israel kufanya jinai kubwa dhidi ya Waislamu ndani ya Msikiti wa al Aqsa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco imemwita balozi wa utawala wa Kizayuni mjini Rabbat ili kumkabidhi wasiwasi wa nchi hiyo kuhusu jinai za Wazayuni katika Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu na ililaani jinai hiyo.

Ijumaa ya tarehe 15 Aprili, wanajeshi makatili wa Israel waliuvamia Msikiti wa al Aqsa huko Palestina na eneo hilo takatifu kwa Waislamu wote duniani lilishuhudia jinai kubwa kuwahi kufanywa na Wazayuni katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Maandamano ya kuiunga mkono Palestina nchini Morocco

 

 

Katika uvamizi huo makumi ya Waislamu wa Palestina waliokuwa wanafanya ibada walijeruhiwa na mamia ya wengine walitekwa nyara na wanajeshi wa Israel. Taarifa zinasema kuwa, Wapalestina wasiopungua 400 walitekwa nyara na wanajeshi hao wa Kizayuni katika uvamizi huo.

Licha ya serikali ya Morocco kujipendekeza kwa Wazayuni na kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala huo pandikizi, lakini wananchi wa Morocco wako pamoja na wananchi wa Palestina na hawaridhishwi hata kidogo na hatua ya nchi yao ya kujidhalilisha kiasi chote hicho kwa Wazayuni. Mara kwa mara wananchi wa Morocco wanafanya maandamano ya kupinga Israel na kuunga mkono Palestina.

Tags