Apr 24, 2022 08:01 UTC
  • Zaidi ya 100 waaga dunia katika mripuko kwenye kiwanda cha mafuta Nigeria

Watu zaidi ya 100 wamepoteza maisha katika mripuko uliotokea katika kiwanda kimoja cha kusafisha mafuta ghafi kusini mwa Nigeria.

Goodluck Opiah, Kamisha wa Rasilimali za Petroli katika jimbo la Rivers eneo la Niger Delta amesema mripuko huo ulitokea usiku wa kuamkia jana Jumamosi, na kwamba wengine zaidi ya 100 wamepata majeraha mabaya ya kuungua na moto kwenye ajali hiyo.

Amesema kiwanda hicho kilikuwa kinafanya kazi kinyume cha sheria. Kwa mujibu wa tovuti ya kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar ni kuwa, kuna makumi ya viwanda haramu vya kusafisha mafuta katika eneo la Niger Delta.

Ukosefu wa ajira umewasukuma vijana wengi kufanya kazi katika mashirika hayo ya kusafisha mafuta ghafi yanayoendeshwa kinyume cha sheria na bila kuzingatia usalama wa wafanyakazi.

Miripuko ya malori na mabomba ya kusafirishia mafuta na gesi huripotiwa mara kwa mara Nigeria

Oktoba mwaka jana, watu 25 wakiwemo watoto wadogo kadhaa waliaga dunia katika mripuko mwingine uliokotokea katika kiwanda haramu cha kusafisha mafuta katika jimbo hilo hilo la Rivers eneo la Niger Delta, kusini mwa Nigeria.

Miripuko ya malori na mabomba ya kusafirishia mafuta na gesi imekuwa ikiripotiwa mara kwa mara nchini Nigeria, taifa la Afrika magharibi lenye utajiri wa bidhaa hizo.

Tags