Apr 27, 2022 03:48 UTC
  • Watu 200 wauawa katika jimbo la Darfur, jeshi la Sudan linatuhumiwa kuhusika

Zaidi ya watu 200 wameuawa huko Darfur, magharibi mwa Sudan kwenye mpaka wa nchi hiyo na Chad, katika mapigano mapya ambayo yalianza hapa na pale katika eneo hilo na baadaye yakageuka kuwa mapigano makali.

Milio ya risasi inaendelea kusikika katika maeneo mengi ya jimbo hilo huku pande zinazozozana zikitumia silaha nzito; hali ambayo imezua hali ya taharuki na wasiwasi miongoni mwa wakazi waliobaki majumbani mwao. Masoko na maduka yote yamefungwa katika mji mkuu wa jimbo hilo, El Geneina.

Mzozo na mapigano ya umwagaji damu katika eneo hilo la Magharibi mwa Sudan kwa kawaida huanza kutokana na ugomvi wa umiliki wa ardhi au mzozo kati ya watu wa makabila tofauti ambao baadaye hugeuka na kuwa mapigano ya kikabila.

Cheche za mapigano ya sasa huko Darfur zilianza Ijumaa iliyopita wakati wachungaji wawili wa makabila ya Kiarabu walipouawa na watu wawili wa kabila la Masalit. Mauaji hayo yalijibiwa kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi na kusababisha ghasia kubwa baila ya makabila hayo mawili. 

Ripoti zinasema, hadi sasa mapigano hayo ya kikabila yamepelekea kuuliwa zaidi ya watu 200 na kwamba shambulio kali zaidi limelenga vijiji vya eneo la Krink, yapata kilomita 80 kutoka mji wa Geneina, wakati makundi ya makabila ya Kiarabu yalipovamia wakazi ya raia kwa kutumia silaha nzito, magari, wanyama na pikipiki, na kuchoma moto nyumba za watu. 

Darfur - Sudan

Raia wa Jimbo la Darfur Magharibi wanaeleza kuwa Kikosi cha Msaada wa Haraka cha Jeshi la Sudan kilingilia mzozo huo kikiwa na zana  nzito za kijeshi kuwasaidia wapiganaji wa makabila ya Waarabu dhidi ya wale wa kabila la Kiafrika la Masalit.

Mzozo wa kugombania ardhi baina ya makabila ya Waarabu na wasio Waarabu katika eneo lenye milima mingi la Jebel Moon mkoa wa Darfur Magharibi umesababisha mapigano ya umwagaji damu na mauaji ya mamia ya watu tokea Novemba mwaka jana hadi sasa.

Eneo la Darfur mwaka 2003 lilikumbwa na mapigano ya umwagaji damu kati ya serikali ya wakati huo ya Sudan chini ya uongozi wa eais aliyeondolewa  madarakani, Omar Hassan al-Bashir, na wapinzani wa serikali.

Umoja wa Mataifa unasema watu wasiopungua 300,000 wameuwa na wengine milioni 2.5 wamelazimika kukimbia makazi yao, kutokana na machafuko ya Darfur.

Tags