May 01, 2022 04:10 UTC
  • UNHCR yahitaji dola milioni 47.8 kuwasaidia wakimbizi Uganda

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR na wadau wengine 44 wa misaada ya kibinadamu wametoa ombi la dharura la dola za Marekani milioni 47.8 ili kukabiliana na mahitaji muhimu ya maelfu ya wakimbizi waliofika Uganda mwaka huu, wakikimbia ghasia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na za mapigano ya hapa na pale nchini Sudan Kusini.

Tangu Januari mwaka huu, Uganda imepokea kwa ukarimu zaidi ya wakimbizi 35,000 ambapo theluthi moja kati yao wamewasili katika muda wa wiki tatu tu zilizopita kutoka DRC, wakikimbia mapigano makali katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri. 

Huku ripoti za ghasia mashariki mwa DRC na Sudan Kusini zikiendelea kutolewa, ombi hili pia litaimarisha uwezo wa Uganda kupokea wakimbizi zaidi endapo watahama zaidi. 

UNHCR inashirikiana na serikali ya Uganda na washirika wa kibinadamu kutoa msaada wa dharura na ulinzi kwa wakimbizi walio katika maeneo ya mpakani, na inafanya jitihada za kuwahamisha kwenye makazi ya wakimbizi haraka iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa shirika la UNHCR mahitaji yanaongezeka kuhusu ulinzi, chakula, malazi na vifaa muhimu vya nyumbani. 

Ufadhili huo pia utasaidia vifaa vya afya vinavyohitajika haraka, pamoja na huduma za maji, vyoo na usafi ambazo ni muhimu ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19 na magonjwa mengine.

Uganda tayari inahifadhi zaidi ya wakimbizi milioni 1.5 idadi kubwa zaidi ya wakimbizi katika bara la Afrika na sasa inapokea maelfu ya wakimbizi wapya kutoka Sudan Kusini, kwenye jimbo la Nile Magharibi hadi eneo la kaskazini, na DRC, wanaowasili kusini magharibi mwa Uganda. 

Ombi la dharura kwa ajili ya Uganda linakusudiwa kuunga mkono juhudi zilizoratibiwa na za dharura kwa ajili ya kudhibiti wimbi la wakimbizi 60,000 nchini Uganda katika nusu ya kwanza ya 2022, na wakimbizi wapya 45,000 wanaotazamiwa kuwasili nchini baadaye mwaka huu.

 

Tags