May 03, 2022 04:43 UTC
  • Watu 8 wameaga dunia baada ya jengo la ghorofa tatu kuporomoka Lagos, Nigeria

Watu wasiopungua 8 wamepoteza maisha baada ya jengo la ghorofa tatu kuporomoka katika jimbo la Lagos nchini Nigeria.

Mratibu wa Kitengo cha Taifa cha Kushughulikia Maafa ya Dharura nchini Nigeria, Ibrahim Farinloye amesema kuwa, hadi sasa maiti nane zimetolewa chini ya vifusi.  

Watu wasiopungua 23 wamenusurika katika ajali hiyo ya kuporomoka jengo la ghorofa tatu huko Lagos na walikuwa wakiendelea kupatiwa matibabu hospitali. Huduma za uokoaji zinaendelea kuona kama kuna watu waliofunikwa chini ya vifusi. 

Ghorofa laporomoka Lagos na kuuwa watu 8 

Tayari uchunguzi umeanza kubaini sababu iliyopelekea nyumba hiyo ya ghorofa tatu kuporomoka na kuuwa watu wasiopungua nane. Mwezi Novemba mwaka jana watu wasiopungua 45 walifariki dunia baada ya jengo la ghorofa 21 kuporopmoka mjini Lagos. Mmiliki wa jengo hilo alikuwa miongoni mwa watu walioaga dunia. 

Kuporomoka majengo ya ghorofa huko Nigeria limekuwa jambo la kawaida, huku wataalamu wa ujenzi wakilaumu masuala kama kutofuata taratibu na kanuni za ujenzi na matumizi ya vifaa visivyo na viwango vya ujenzi, ujenzi mbaya n.k kuwa miongoni mwa sababu za kuporomoka mara kwa mara kwa majengo ya ghorofa nchini Nigeria. 

Kwa mujibu wa mtafiti wa Chuo Kikuu nchini Afrika Kusini, tokea mwaka 2005 hadi sasa, majengo ya ghorofa yasiyopungua 152 yameporomoka mjini Lagos na kusabisha vifo na majeruhi. 

Tags