May 04, 2022 08:09 UTC
  • Watu 11 waugua homa ya Dengi (Dengue) Kodivaa

Wizara ya Afya ya Kodivaa imetangaza kuwa, kesi 11 za homa ya Dengue zimeripotiwa nchini humo; akthari zikiwa Abidjan mji mkuu wa zamani wa nchi hiyo.

Wizara ya Afya ya Kodivaa jana ilitoa taarifa na kusisitiza kuwa, ugonjwa wa homa ya Dengi au Dengue ambao ulitangazwa nchini humo tokea Machi 22 mwaka huu, umeuathiri pakubwa mji wa Abidjan na hadi sasa watu 11 wameugua maradhi hayo na mmoja ameaga dunia.

Homa ya Dengi ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambapo ueneaji wake unafanana na ule wa malaria.  

Homa ya Dengi inaambukizwa na virusi vya mbu aina ya Aedes ambao ni weusi wenye madoadoa meupe yenye kung'aa. Dalili za ugonjwa huo huanza kujitokeza siku tatu mpaka 14 tangu mtu anapoambukizwa.  

Mtu mwenye homa ya Dengi huwa na dalili za homa ya ghafla, kuumwa kichwa, uchovu wa mwili, maumivu ya maungo na misuli, kichefuchefu na kutapika, kuwashwa macho, muwasho na kuwa navipele vidogo vodogo.

Dalili za Homa ya Dengue 

Mwaka 2019 pia Kodivaa ilitangaza kuwa na kesi za homa ya Dengi ambapo watu 130 walipatwa na ugonjwa huo na watu wawili walipoteza maisha kwa homa hiyo. 

Tags