May 04, 2022 14:54 UTC
  • Ajali ya basi yasababisha vifo vya watu wasiopungua 20 nchini Uganda

Polisi wa Uganda wamesema watu 20 wameuawa baada ya basi la abiria kuanguka kwenye shamba la chai nje ya barabara kuu magharibi mwa Uganda.

Polisi wamesema takriban saba kati ya walioaga dunia katika ajali hiyo iliyotokea mapema leo Jumatano katika eneo la Ssebitoli Wilayani Kabarole ni watoto.

Hakukuwa na taarifa za haraka kuhusu kilichosababisha ajali hiyo ambayo imetajwa kuwa miongoni mwa ajali mbaya zaidi nchini Uganda katika miaka ya hivi karibuni.

Basi hilo lilikuwa likisafiri kutoka mji wa Fort Portal kuelekea mji mkuu wa Uganda, Kampala.

Picha kutoka eneo la tukio zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha watu wakijaribu kuwaokoa manusura kutoka kwenye mabaki ya basi hilo.

Ajali mbaya za magari hutokea mara kwa mara nchini Uganda, ambako barabara kuu ni nyembamba na mara nyingi zimejaa mashimo. Ajali za kugongana magari uso kwa uso zinazohusisha magari makubwa, zimekuwa jambo la kawaida nchini Uganda.

Tags