May 05, 2022 05:30 UTC
  • Shambulio la kundi la kigaidi la as-Shabaab dhidi ya askari wa kulinda amani nchini Somalia

Jeshi la Burundi limetangaza kuwa askari wake 10 wa kulinda amani wanaohudumu nchini Somalia chini ya mwavuli wa Umoja wa Afrika wameuawa katika shambulio lililotekelezwa na kundi la kigaidi la as-Shabaab katika kambi ya askari wa umoja huo.

Tangu kuasisiwa kundi hilo la kigaidi mwaka 2004 serikali ya Somalia imekuwa ikipambana na kundi hilo ambalo limesababisha malefu ya watu kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Kundi hilo kimsingi hulenga askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, na vilevile kuhusika na mashambulio ya umwagaji damu katika maeneo mengine ya Afrika na hasa Afrika Mashariki.

Jeshi la Burundi limetangaza kuwa katika shambulio lililotekelezwa na kundi hilo Jumanne, askari wengine 25 walijeruhiwa, watano wakatoweka na magaidi 20 pia wakauawa.

Askari wa Umoja wa Afrika nchini Somalia

Hii ni katika hali ambayo Radio Andalus inayofungamana na as-Shabaab imedai katika propaganda zake kuwa katika shambulizi hilo askari 173 wa Burundi waliuawa

Wakati huo huo Moussa Faki Mahamat, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ametoa taarifa akilaani vikali hujuma hiyo ya as-Shabaab na kusisitiza kuwa shambulio hilo la kigaidi halitaathiri kwa namna yoyote ile azma ya umoja huo ya kuendelea kuunga mkono serikali na watu wa Somalia. Askari wa Umoja wa Afrika wanalinda amani huko Somalia kwa uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa ambapo askari wapatao 20,000 kutoka Uganda, Ethiopia, Burundi na Kenya wanahudumu katika kikosi hicho.

Tags