May 06, 2022 12:11 UTC
  • Raia mwingine auawa na vikosi vya usalama katika maandamano nchini Sudan

Maandamano nchini Sudan yameendelea kushuhudiwa sambamba na ukandamizaji unaofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji ambapo raia mwingine ameuawa katika maandamano hayo.

Kuuawa raia huyo, kunaifanya idadi ya waandamanaji waliouawa nchini Sudan tangu Jeneral Abduul-Fatah al-Burhan afanye mapinduzi ya kijeshi kufikia watu 95.

Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa, kuna haja kwa jamii ya kimataifa kuwashinikiza wanajeshi wanaotawala nchini Sudan ili wakomeshe hatua za kuwakamata kiholela wapinzani na kukiuka haki za wanaharakati wanaopinga mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea mwaka uliopita.

Omar al Bashir aliyetawala Sudan kwa miongo mitatu alipinduliwa Aprili 2019 na Agosti mwaka huo huo utawala wa mpito wa jeshi na raia uliteuliwa kushika hatamu za uongozi. Hata hivyo mkuu wa majeshi ya Sudan, Abdul-Fattah al-Burhan ambaye alikuwa ameteuliwa kuwa rais, alipindua serikali Oktoba mwaka jana na kuwatimua raia serikalini.

Maandamano ya wananchi wa Sudan

 

Waziri Mkuu Abdallah Hamdok ambaye alikuwa anaongoza mrengo wa raia katika serikali ya Sudan alikamatwa na kisha kuachiliwa huru.

Mapinduzi hayo yaliibua maandamano makubwa na yalilaaniwa kimataifa. Sudan, yenye idadi ya watu milioni 45 inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi ambapo mfumuko wa bei sasa umefika asilimia 400.

Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, hadi sasa watu zaidi ya 130 wameuawa nchini Sudan katika maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi nchini humo.

Tags