May 09, 2022 10:57 UTC
  • Algeria kufuatilia jinai za Ufaransa nchini humo wakati wa ukoloni

Rais wa Algeria amekosoa vikali mauaji ya kimbari yaliyotokelezwa dhidi ya taifa hilo na dola la kikoloni la Ufaransa na kuongeza kuwa, Algeria itafuatilia faili la jinai za Ufaransa nchini humo katika zama za ukoloni na kuwa haiko tayari kufanya muamala kuhusu kadhia hiyo.

Rais Abdelmadjid Tebboune ameyasema hayo katika ujumbe ambao ameutuma kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mauaji ya Mei 8 mwaka 1945 ambayo yalitekelezwa na Ufaransa na kusisitiza kuwa, jinai hiyo ingali hai katika fikra za Waalgeria. Amesema katu haiwezekani kusahau mauaji ya kinyama yaliyotekelezwa na Ufaransa katika kipindi hicho.

Ikumbukwe kuwa katika kipindi hicho, wanajeshi vamizi wa Ufaransa waliwashambulia waandamanaji wa Algeria waliokuwa wakilalamikia ukoloni katika maeneo ya Satif, Qaimah na Khratah. Kwa mujibu wa takwimu rasmi, watu 45,000 waliuawa na askari wa Ufaransa katika jinai hiyo na kosa lao lilikuwa ni kutaka uhuru.

Katika miaka ya hivi karibuni Algeria imekuwa ikiitaka Ufaransa ikiri kuhusu jinai ambazo ilizitenda wakati wa ukoloni na iombe msamaha sambamba na kulipa fidia. 

Hata hivyo Ufaransa imekuwa ikidai kuwa yaliyopita yasahaulike na kwamba mustakabali ndio muhimu. 

Oktoba mwaka jana serikali ya Algeria ilimwita nyumbani balozi wake wa Ufaransa kwa ajili ya mashauriano ikilalamikia matamshi yaliyotolewa na Rais Emmanuel Macron dhidi ya nchi hiyo ambayo Algiers imeyataja kama ya upotoshaji na uingiliaji masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Rais Abdelmadjid Tebboune

Jarida la kila siku la Ufaransa, Le Monde lilimnukuu Emmanuel Macron akidai kwamba, historia ya Algeria haijajengeka katika msingi wa ukweli na uhakika bali imejengeka juu ya misingi ya maneno ya chuki dhidi ya Ufaransa.

Matamshi hayo ya Macron yaliikasirisha mno serikali ya Algeria ambayo ilichukua uamuzi wa kumrejesha nyumbani balozi wake wa mjini Paris Ufaransa, hatua ambayo huenda ikawa ni ishara ya kulegalega zaidi uhusiano wa nchi mbili hizo.

Algeria ilikoloniwa na Ufaransa kwa muda wa miaka 132.

Vita vya uhuru wa Algeria vilianza mwaka 1954 hadi 1962 ambapo zaidi ya Waalgeria milioni moja na nusu waliuawa katika ukandamizaji uliokuwa ikitekelezwa na askari wa Ufaransa.

Tags