May 12, 2022 02:21 UTC
  • Wagombea 39 kuwania kiti cha urais nchini Somalia

Wagombea wapatao 39 wamejitokeza kuwania kiti cha urais nchini Somalia uchaguzi ambao umepangwa kufanyika mwishoni mwa juma hili.

Kamati ya bunge iliyopewa jukumu la kusimamia uchaguzi huo uliocheleweshwa kwa muda mrefu imetangaza kuwa, wagombea 39 wamejitokeza kuwania urais katika nchi hiyo inayokabiliwa na ukosefu wa usalama.

Miongoni mwa wagombea waliojitokeza wamo marais wawili wa zamani, Hassan Sheikh Mohamud aliyeongoza kati ya 2012 na 2017, Sharif Sheikh Ahmed, aliyeongoza kati ya 2009 na 2012, vile vile waziri mkuu wa zamani, Hassan Ali Khaire aliyehudumu kwenye uadhifa huo kati ya 2017 na 2020.

Wabunge na maseneta watamchagua rais mpya ndani ya jengo la uwanja wa ndege wa Mogadishu wenye ulinzi mkali katika nchi hiyo ambayo inapambana na uasi wa wanamgambo wa kundi la al-Shabab.

 

Kamati ya Bunge la Somalia inayoshughulikia masuala ya uchaguzi imetangaza kuwa, uchaguzi wa rais nchini humo utafanyika Jumapili ijayo Mei 15 mwaka huu baada ya kuchelewesha kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Uchaguzi huo utafanyika baada ya kucheleweshwa kwa mwaka mmoja ikiwa ni kinyume na ilivyokuwa imepangwa hapo awali, baada ya mchakato wa maandalizi ya uchaguzi kukumbwa na ghasia pamoja na mzozo wa kuwania madaraka kati ya Rais Mohamed Abdullahi Mohamed, maarufu Farmajo, na Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble.

Matatizo ya kisiasa nchini Somalia yaliongezeka baada ya Rais Mohamed Abdullahi Mohamed kujaribu kuongeza muda wake kwa miaka miwili zaidi baada ya muhula wa miaka minne kumalizika, hatua ambayo ilipingwa na Bunge.

Tags