May 16, 2022 02:26 UTC
  • Wakili wa Seif al-Islam Gaddafi: Marekani na Uingereza zilivuruga uchaguzi wa Libya

Wakili wa Seif al-Islam Gaddafi amefichua kuwa, mabalozi wa Marekani na Uingereza nchini Libya ndio waliofanya njama za kuvuruga uchaguzi wa Libya na hivyo kupelekea kuakhirishhwa.

Khalid al-Zaydi, wakili wa Seif al-Islam mwana wa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la al-Mirsad la Libya na kueleza kwamba, kwa mujibu wa nyaraka na ushahidi alionao ni kuwa, baada ya Seif al-Islam kutangaza nia ya kugombea urais na hata kutimiza masharti, mabalozi wa Marekani na Uingereza waliingilia mwenendo wa uchaguzi huo na kuuvuruga.

Ameongeza kuwa, sababu ya njama za mabalozi hao wa Marekani na Uingereza ni hofu waliyokuwa nayo ya kushinda Seif al-Islam Gaddafi katika uchaguzi huo.

Seif al-Islam Gaddafi

 

Huko nyuma Richard Norland, balozi wa Marekani nchini Libya aliwahi kunukuliwa akisema kuwa, kuingia Seif al-Islam Gaddafi katika kinyang'anyiro cha kuwania kiti cha urais ni mithili ya bomu ambalo liko ndani ya chumba lenye uwezo wa kulipuka wakati wowote na kuharibu kila kitu.

Aidha alisema kuwa, Seif al-Islam hana sifa za kugombea urais na kwamba anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa kutenda jinai.

Libya imetumbukia katika mgogoro wa kisiasa kutokana na kukosekana umoja miongoni mwa taasisi ya jeshi na nafasi za uongozi wa serikali na sasa nchi hiyo iko katika ombwe la kisiasa kwa sababu ya hitilafu za mitazamo kati ya makundi ya ndani.