May 16, 2022 03:34 UTC
  • Hassan Sheikh Mohamud achaguliwa kuwa rais mpya wa Somalia

Wabunge nchini Somalia wamemchagua rais wa zamani Hassan Sheikh Mohamud kuwa rais mpya wa nchi hiyo baada ya upigaji kura uliodumu siku nzima katika bunge la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Hassan Sheikh Mohamud, ambaye alikuwa rais wa Somalia kuanzia 2012 hadi 2017, alimshinda rais anayeondoka Mohamed Abdullahi Mohamed,  maarufu kama Farmajo katika uchaguzi huo uliofanyika katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, huku kukiwa na usalama mkali kuzuia hujuma za kigaidi.

Baada ya upigaji kura uliokuwa na wagombea 36 na kutangazwa mubashara kupitia televisheni, Mohamud alipata kura 214 kati ya kura 327 zilizopigwa na wabunge huku Farmajo akipata kura 110, alitangaza Spika wa Bunge Adan Mohamed Nur ambaye aliongeza kuwa kura tatu ziliharibika.

Mohamud mwenye umri wa miaka 66 ni kutoka ukoo wa Hawiye ambao ni kati ya koo kubwa Somalia na ni mashuhuri kwa kazi yake ya kustawisha elimu Somalia hasa kuanzisha Chuo Kikuu cha SIMAD mjini Mogadishu.

Kwa muda wa miaka 50 sasa wananchi wa Somalia hawajawahi kushiriki katika uchaguzi wa moja kwa moja wa Rais.

Mohamed Abdullahi Mohamed, maarufu kama Farmajo

Jana pia rais alipigiwa kura na wajumbe katika mabunge mawili. Bunge la Juu na Bunge la Chini ndio waliopiga kura ya siri kumchagua rais. Wabunge hao nao pia hawakuchaguliwa kwa kura za moja kwa moja za wananchi bali walichaguliwa kwa kura za wajumbe kutoka majimbo ya nchi hiyo.

Farmajo alimpongeza Mohamud kufuatia ushindi huo na pia aliwashukuru wote waliompigia kura na wale ambao hawakumbikia kura.

Punde baada ya kutangazwa mshindi Mohamud aliapishwa ambapo amemshukuru Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble kwa kuongoza mchakato wa uchaguzi.