May 16, 2022 08:08 UTC
  • Mali yajitoa katika kundi la nchi tano za Sahel, G5

Jeshi la Mali limetangaza kujitoa nchi hiyo katika kundi la nchi tano za eneo la Sahel linalojulikana kama G5 ambalo lilibuniwa mwaka 2014

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, jeshi tawala nchini Mali limesema katika taarifa iliyotangazwa Jumapili jioni kwamba serikali imeamua kujiondoa katika vyombo na idara zote za Kundi la G5, ikiwa ni pamoja na vikosi vya pamoja vya kupambana na makundi ya kigaidi. Kundi hilo lililoundwa mwaka wa 2014, lilizindua kikosi chake cha pamoja cha kukabiliana na ugaidi mwaka 2017.

Tangazo hilo linakuja wakati ambao Bamako awali ilipangiwa kuwa mwenyeji wa kikao cha viongozi wa Sahel mwezi Februari mwaka huu, lakini mkutano huo umeakhirishwa na haujafanyika kwa takriban miezi mitatu sasa.

Kufuatia mapinduzi ya 2020 na 2021 ambayo yalifanyika katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja, Mali, kwa miaka kadhaa sasa tangu Januari 9, imekuwa chini ya vikwazo vikali vya kiuchumi na kidiplomasia, haswa kutoka kwa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS),  kutokana na hatua ya Baraza la Kijeshi la nchi hiyo, ya kuendelea kung'ang'ania madaraka.

Kanali Assimi Goita, kiongozi wa kijeshi wa Mali

Mali imekuwa katika mzozo wa usalama tangu 2012, na vikosi vya kigeni vimeshindwa kurejesha usalama nchini humo.

Mali na baadhi ya nchi jirani zimekuwa kitovu cha makundi ya kigaidi. Ukosefu wa usalama katika eneo hilo unashuhudiwa katika hali ambayo Ufaransa imekuwepo kijeshi nchini Mali kwa miaka mingi, ikidai kuwa inapambana na ugaidi.