May 17, 2022 11:46 UTC
  • Mwenyekiti wa AU kuzuru Russia na Ukraine ili kufuatilia udhamini wa nafaka

Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU) Rais Macky Sall wa Senegal atafanya ziara hivi karibuni katika nchi za Russia na Ukraine ili kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hizo kuhusiana na kudhaminiwa bara la Afrika nafaka na mbolea ya kemikali.

Russia na Ukraine zinadhamini karibu theluthi nzima ya ngano duniani huku Ukraine peke yake ikiwa inasafirisha asilimia 12 ya ngano kwenye masoko ya dunia kabla ya kutokea vita na mapigano kati ya nchi hiyo na Russia.

Tangu vilipoanza vita na mapigano kati ya nchi hizo mbili, bei ya ngano katika soko la dunia imepanda kutokana na hofu kupungua kiwango cha mauzo ya bidhaa hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, Mwenyekiti wa AU Macky Sall amesema: "Tumekabidhiwa mamlaka na Umoja wa Afrika ya kumtaka Rais Vladimir Putin wa Russia aandae mazingira na kuiruhusu Ukraine isafirishe nafaka na mbolea tunazohitaji. Vilevile tufanye mazungumzo kuhusiana na uwezekano wa kuondolewa baadhi ya vikwazo dhidi ya Russia ili kuwepo na wepesi kwa sisi kufanya biashara na kudhaminiwa mbolea."

Rais huyo wa Senegal ameyasema hayo siku ya Jumatatu katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa 54 wa mawaziri wa fedha na uchumi wa nchi za Afrika uliofanyika katika mji wa Diamniadio nchini humo.

Sall ameongezea kwa kusema, anataka kupunguzwa mivutano nchini Ukraine na kwamba Afrika iko kwenye kitovu cha waathirika wa vita na mapigano yanayoendelea nchini humo huku, ikiwa haina uwezo wa kufanya lolote kuhusiana na hali hiyo.../