May 18, 2022 03:54 UTC
  • Mapigano yaripotiwa Tripoli baada ya kuwasili mpinzani aliyejitangaza waziri mkuu

Waziri mkuu aliyeteuliwa na bunge la Libya alijaribu kwa muda mfupi kuchukua mji mkuu wa Tripoli kabla ya kulazimishwa kuondoka saa chache baada ya kuwasili kwake kusababisha mapigano kati ya wanamgambo wa mirengo hasimu.

Mapigano yalizuka mapema Jumanne asubuhi wakati Fathi Bashagha alijaribu kuchukua udhibiti wa serikali kutoka kwa utawala hasimu unaotambuliwa na Umoja wa Mataifa wa Abdel Hamid Dbeibeh, ambao umekataa kuachia madaraka.

Bashagha, ambaye aliteuliwa kuwa waziri mkuu na bunge lenye makao yake mjini Tobruk mwezi Februari, aliingia Tripoli Jumatatu usiku baada ya miezi miwili ya mvutano kati ya tawala hasimu za Libya, lakini akajiondoa saa chache baadaye huku mapigano yakiutikisa mji mkuu, kwa ajili ya "kulinda usalama na usalama wa raia" , ofisi yake ilisema.

Milio ya silaha nzito na risasi ilisikika katika mji mkuu Jumanne asubuhi na kusababisha shule kufungwa.

Libya imekuwa na serikali mbili tangu Baraza la Wawakilishi lenye makao yake makuu mjini Tobruk mashariki mwa nchi hiyo kumteua Bashagha kuwa waziri mkuu.

Nchi hiyo ya Afrika Kaskazini imekumbwa na mgawanyiko tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipozuka mwaka 2014 kati ya tawala hasimu zilizoko magharibi na mashariki mwa nchi hiyo. Vita hivyo viliisha mwaka 2020, lakini migawanyiko imebakia.

Watu wengi wanamwona Bashagha kuwa muitifaki wa jenerali muasi Khalifa Haftar, kamanda wa kijeshi aliyeko mashariki mwa nchi ambaye alianzisha hujuma ya kijeshi ya miezi 14 huko Tripoli mnamo 2019.

Abdel Hamid Dbeibeh (kushoto) na Fathi Bashagha

Mshauri maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya Stephanie Williams, alitoa wito wa kuwepo utulivu na pande zinazohasimiana kujizuia kushiriki katika mapigano hayo.

Dbeibah hapo awali alisema ataiachia tu mamlaka serikali ambayo itaingia madarakani kupitia "bunge lililochaguliwa na wananchi", na hivyo kuzua hofu kwamba nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta inaweza kurejea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wabunge wamesema kuwa muda wa Dbeibah ulimalizika baada ya Libya kushindwa kufanya uchaguzi wa rais mwezi Disemba kama ilivyopangwa chini ya makubaliano ya Umoja wa Mataifa.

Nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta imekuwa ikikumbwa na mzozo tangu uasi ulioungwa mkono na NATO kumwangusha na kumuua dikteta wa muda mrefu Muammar Gaddafi mwaka 2011.