May 18, 2022 08:01 UTC
  • Muhoozi Kainerugaba: Uganda kuondoa majeshi yake mashariki mwa DRC

Uganda imetangaza kuwa, itawaondoa wanajeshi wake waliokko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Hayo yameelezwa na Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, Kamanda wa jeshi la nchi kavu la Uganda ambaye amebainisha kwamba, Operation Shujaa ambayo ilitakiwa kudumu kwa miezi sita itafikia kikomo rasmi takriban wiki mbili zijazo.

Muhoozi Kainerugaba ambaye ni mtoto wa rais wa Uganda Yoweri Museveni na ambaye amekuwa akitajwa kumrithi baba yake amesema kwamba, kama hatapata maelekezo zaidi kutoka kwa Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Uganda au mnadhimu wa jeshi basi atawaondoa wanajeshi wote wa nchi hiyo walioko mashariki mwa Jamhurii ya Kidemokrasia ya Congo.

Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, Kamanda wa jeshi la nchi kavu la Uganda

 

Serikali ya Uganda iliwapeleka mamia ya wanajeshi mashariki mwa Congo mwezi Desemba mwaka uliopita kwa ajili ya kulisaidia jeshi la nchi hiyo kuzishambulia kambi za kundi la waasi wa Allied Democratic Forces ADF.  

Kwa muda mrefu, kundi hilo la kigaidi limekuwa likipinga utawala wa Rais Yoweri Museveni, kiongozi wa muda mrefu wa Uganda ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa Kiafrika kutuma askari wa kulinda amani nchini Somalia ili kuihami serikali kuu ya nchi hiyo dhidi ya hujuma za kundi la kigaidi la al-Shabab.

Wanamgambo wa ADF wanahesabiwa kuwa ni waasi makatili zaidi huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri yamekuwa yakishuhudia mashabulizi ya mara kwa mara ya kikatili ya waasi hao.