May 18, 2022 12:50 UTC
  • Maoni: Raila amempiku Ruto katika urais Kenya kwa kuteua mgombea mwenza mwanamke

Umaarufu wa kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais umeongezeka kwa asilimia tatu na kufikia asilimia 39 dhidi ya mpinzani wake mkuu naibu rais wa taifa hilo, William Ruto, ambaye umaarufu wake umepungua kutoka asilimia 39 na kufikia asilimia 35.

Hayo ni kwa mujibu wa zoezi la uchunguzi wa maoni lililoendeshwa na shirika la utafiti la TIFA, ambao unaonyesha kuwa, umaarufu wa Odinga umeongezeka kutokana na hatua yake ya kumteua mgombea mwenza mwanamke, aliyekuwa Waziri wa Sheria Martha Karua.

Utafiti huo uliohusisha Wakenya 1,719 ambao walihojiwa kupitia njia ya simu ulifanywa jana tarehe 17 Mei, siku moja baada ya Odinga kumtangaza Bi Karua kuwa mgombea wake mwenza na siku mbili baada ya Ruto kumteua Rigathi Gachagua katika nafasi hiyo.

Odinga ambaye aliwahi kuhudumu kama waziri mkuu nchini Kenya, katika uchunguzi wa maoni uliofanywa mwezi Aprili, alikuwa na asilimia 32 ya umaarufu akitanguliwa na Ruto aliyekuwa na asilimia 39 wakati huo.

William Ruto, (kulia) na Raila Odinga

Pamoja na hayo, utafiti uliofanywa na TIFA umebaini kuwa, hadi sasa hakuna chama chochote cha siasa ambacho kimeweza kuvutia uungaji mkono wa zaidi ya theluthi moja ya Wakenya. Chama cha naibu rais William Ruto cha United Democratic Alliance, UDA, kinaongoza kwa umaarufu kwa asimilia 29 dhidi ya kile cha Raila Odinga cha Orange Democratic Movement, ODM kinachokubalika kwa asilimia 25.

Halikadhalika, kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni, ukiondoa idadi ndogo kabisa ya asilimia tatu, katika watu waliotoa maoni yao ambao walijitambulisha kama waungaji mkono wa chama tawala cha Jubilee, katika idadi inayozidi kidogo theluthi moja ambayo ni asilimia 37, asilimia 18 miongoni mwao wamesema bado hawajachagua chama watakachokiunga mkono, asilimia 13 wamesema hawana chama chochote na asilimia sita wamekataa kujibu suali kuhusu uungaji mkono wao kwa vyama vya siasa.

Uchaguzi wa urais nchini Kenya unatarajiwa kufanyika Agosti 9 mwaka huu, huku kipindi cha kampeini kikitarajiwa kuanza mwisho wa mwezi huu.../

 

 

 

 

Tags