May 18, 2022 13:51 UTC
  • Mkuu wa MOSSAD alifukuzwa 'kimbwa kinguruwe' Kongo DR na Rais wa nchi hiyo Tshisekedi

Gazeti la Kizayuni la Haaretz limefichua kuwa mwaka 2019, Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alimfukuza nchini humo 'kimbwa kinguruwe' mkuu wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel, Yossi Cohen katika kile kinachoelezwa kama kashfa ambayo haijawahi kushuhudiwa katika historia ya utawala huo bandia.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilimtimua nchini humo kiudhalilishaji mkuu huyo wa Mossad kutokana na safari zake za mara kwa mara zilizokuwa zikitiliwa shaka huku akiandamana na bilionea wa Kizayuni aitwaye Dan Gertler.

Licha ya vizuizi na uchujaji wa taarifa unaofanywa na mfumo wa uangalizi wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni, gazeti mashuhuri la Kizayuni la Haaretz limeweza kunasa na kutangaza baadhi ya taarifa kuhusu kufukuzwa kimadhila nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyekuwa mkuu wa shirika la ujasusi la Israel wakati huo Mossad, Yossi Cohen.

Ripoti ya gazeti hilo imebainisha kuwa, Cohen alifanya safari mara tatu DRC bila kuwasiliana na maafisa wa nchi hiyo, lakini katika safari yake ya tatu, rais Felix Tshisekedi alimwamuru mkuu huyo wa Mossad aondoke na kumtaka asikanyage tena ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa baadhi ya duru, wakati Cohen alipokuwa nchini Kongo DR alikuwa akiwasiliana na Joseph Kabila, rais wa zamani na mpinzani mkuu wa Tshisekedi na kwamba akila njama ya kuandaa mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ya nchi hiyo.

Haaretz limefafanua kuwa, Yossi Cohen alikuwa akifanya safari nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa siri na kwamba kulingana na sheria za mfumo wa uangalizi wa kijeshi ni marufuku kuzungumziwa hadharani safari hizo.

Shirika la ujasusi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel MOSSAD limekuwa likijipenyeza na kuendesha harakati zake katika baadhi ya nchi za Kiafrika kwa lengo la kupanua wigo wa satua na ushawishi wake barani humo.

Harakati za utawala haramu wa Israel katika bara la Afrika zimekithiri mpaka ikafika hadi mwaka uliopita mkuu wa kamisheni ya Umoja wa Afrika AU Moussa Faki akatangaza kupatiwa utawala huo bandia hadhi ya mwanachama mtazamaji katika umoja huo.

Hata hivyo njama hiyo ya utawala wa Kizayuni iligonga mwamba baada ya kusimamishwa utekelezaji wa uamuzi huo kutokana na upinzani wa nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Afrika zikiongozwa na Algeria.../