May 19, 2022 12:40 UTC
  • HRW yavituhumu vyombo vya dola Burundi kwa ukiukaji wa haki za binadamu

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, limesema maafisa wa usalama nchini Burundi wamehusika na dhulma dhidi ya raia wanaoshukiwa kuegemea upande wa upinzani, au kushirikiana na makundi ya watu wenye silaha.

Katika ripoti yake mpya, Human Rights Watch imewahusisha polisi, idara ya ujasusi na vijana wanaogemea chama tawala kuwashumbulia raia na idara za serikali.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema mamlaka nchini Burundi haijaonyesha nia yoyote ya kuendesha uchunguzi huru, ili kuwachukulia hatua wanaohusishwa na vitendo hivyo vya ukiukaji wa haki za binadamu.

Mtafiti mkuu wa HRW kanda ya Africa, Clémentine de Montjoye, ameitaka serikali ya Rais Everiste Ndayishimiye, iwachukulie hatua za kisheria maafisa wa usalama wanaohusishwa  na vitendo hivyo vya dhulma, badala ya kuwalenga wapinzani wake.

Rais Everiste Ndayishimiye wa Burundi

Montjoye amesema raia wa Burundi wataacha kuishi na uoga pale serikali itakapowawajibisha wanaohusika na vitendo hivyo.

Human Rights Watch imesema ripoti yake imetegemea ushahidi wa raia 30 wa Burundi, wakiwemo wafuasi wa vyama vya upinzani na watetezi wa haki za binadamu, kupitia uchunguzi iliofanya kati ya Oktoba  2021 hadi April 2022.

Mashirika ya kiraia pia yamesema yamejionea kanda za video ambazo polisi na wanajeshi walikiri kuhusika na mauaji ya raia.

HRW kadhalika imeukosoa Umoja wa Ulaya, Marekani na mataifa mengine kuonyesha nia ya kuboresha  uhusiano na Burundi, licha ya ushahidi uliopo wa mamlaka nchini humo kuendelea kukiuka haki za binadamu.../

Tags