May 20, 2022 01:22 UTC
  • Rais mpya wa Somalia ataja vipaumbele katika siku 100 za kwanza za kuwa madarakani

Hassan Sheikh Mohamud, Rais mteule wa Somalia ametangaza vipaumbele vyake katika siku 100 za awali za kuwa kwake madarakani.

Hassan Sheikh Mohamud amesema kuwa, serikali yake itayapa kipaumbele masuala ya usalama, kufufua uchumi uliodorora, uthabiti wa kisiasa, na ahueni ya madeni katika kipindi chake cha siku 100 za kwanza madarakani.

Amesisitiza kuwa: “Tunataka kutekeleza kile tunachotaka kufanya katika siku zangu 100 za kwanza ofisini. Tunataka kufanya mageuzi ya mfumo wa zamani wa kisheria na muundo wa mashirika yetu ya usalama na tunataka kuvishirikisha vyombo vya usalama”.

Kupambana na kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye uhusiano na mtandao wa al-Qaeda ambalo limeshadidisha mashambulizi yake mjini Mogadishu katika miezi ya karibuni ni moja ya changamoto kubwa sana zinazomkabili kiongozi huyo mpya wa Somalia.

Abdullahi Mohamed, maarufu kama Farmajo ambaye ameshindwa na Hassan Sheikh Mohamud katika uchaguzi wa Rais wa 15/05/2022

 

Jumapili iliyopitaa, Wabunge wa Somalia walimchagua rais wa zamani Hassan Sheikh Mohamud kuwa rais mpya wa nchi hiyo baada ya upigaji kura uliodumu siku nzima katika bunge la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Hassan Sheikh Mohamud, ambaye alikuwa rais wa Somalia kuanzia 2012 hadi 2017, alimshinda rais anayeondoka Mohamed Abdullahi Mohamed, maarufu kama Farmajo katika uchaguzi huo uliofanyika katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, huku kukiwa na usalama mkali kuzuia hujuma za kigaidi.