May 20, 2022 08:15 UTC
  • UN yatahadharishwa: Yanayojiri Ethiopia yanaweza kuwa sawa na mauaji ya kimbari ya 1994 Rwanda

Jumuiya 15 za asasi za kiraia barani Afrika zimetahadharisha kuwa yanayojiri katika vita vinavyoendelea hivi sasa nchini Ethiopia yanaweza yakaishia kuwa sawa na mauaji ya kimbari yaliyotokea mwaka 1994 nchini Rwanda ikiwa Umoja wa Mataifa hautachukua hatua haraka za kuuweka mgogoro huo katika ajenda zake.

Katika barua yao kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, asasi hizo 15 za kiraia barani Afrika zimeeleza kwamba, mbali na jinai za vita na jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa na pande zote mbili katika vita vya Ethiopia, maneno kama "saratani" na "shetani" yanayotumiwa kuwaita wanadamu wanaoonekana kuwa wapinzani yanaakisi kile kilichotokea huko nyuma katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Itakumbukwa kuwa serikali ya Rwanda wakati huo iliyokuwa ikiongozwa na watu wa kabila la Wahutu waliowengi ilikuwa ikiwaita Watutsi wa jamii ya wachache "mende" kumaanisha wadudu waharibifu wanaohitaji kuangamizwa.

Sehemu moja ya barua ya asasi za kiraia barani Afrika kwa Baraza la Usalama la UN, ambayo imewasilishwa na Hala Al Karib, mwanaharakati wa haki za wanawake katika Pembe ya Afrika na  eneo la Sudan na Corlett Letlojane, mkurugenzi mtendaji wa  Taasisi ya Haki za Binadamu ya Afrika Kusini imesema: "Miaka 28 iliyopita, sawa na sasa, Baraza la Usalama lilishindwa kubaini ishara za tahadhari za mauaji ya kimbari nchini Rwanda au kuchukua hatua za kuyazuia.

Athari za mauaji ya kimbari ya Rwanda

Barua hiyo imetahadharisha kwa kusema: "Umoja wa Mataifa ulikuwa na nyenzo za kuwezesha kuingilia kati, lakini uliamua kutojali kuingilia itakiwavyo nchini Rwanda. Tuna wasiwasi kuwa hali hiyo inajirudia leo Ethiopia. Tunakutakeni mjifunze kutokana na Rwanda na kuchukua hatua sasa hivi."

Vita vya Ethiopia kati ya vikosi vya jeshi la serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed na vya wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) ambavyo vilianza Novemba 2020 vimesababisha maafa makubwa ya kibinadamu. Vita hivyo vilivyoanzia eneo la Tigray vimesambaa kuelekea kusini hadi eneo la Amhara na mashariki hadi eneo la Afar.

Uchunguzi wa pamoja uliofanywa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na Tume ya Haki za Binadamu ya Ethiopia (EHRC) umebaini kuwa pande zote mbili katika vita hivyo zimehusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Watu wanaokadiriwa kufikia nusu milioni wameshauawa hadi sasa, milioni nne na laki mbili wamebaki bila makazi na milioni tisa wanahitaji misaada ya kibinadamu.../

Tags