May 20, 2022 12:20 UTC
  • Umoja wa Mataifa wasikitishwa na hatua ya Mali ya kujitoa katika kikosi cha kupambana na ugaidi

Umoja wa Mataifa umesikitishwa na uamuzi wa nchi ya Mali ya kujiondoa katika kikosi cha kundi la nchi tano za eneo la Sahel linalojulikana kama G5 ambalo lilibuniwa mwaka 2014 kwa ajili ya kupambana na ugaidi katika eneo hilo.

Bi Martha Pobee, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya siasa barani Afrika ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, uamuzi huo wa Mali unasikitisha mno.

Aidha ameeleza kwamba, hatua ya Mali ya kujiondoa katika kikosi cha mataifa matano ya eneo la Sahel Afrika kilichoundwa kwa ajili ya kupambana na ugaidi ni sawa na kupiga hatua kurudi nyuma hasa katika kipindi hiki ambapo harakati za ugaidi katika eneo hilo zimeongezeka.

Uamuzi wa Mali wa kujiondoa katika kikosi hicho cha pamoja hasa katika kipindi hiki ambao umechukuliwa na utawala wa kijeshi nchini Mali umewashangaza wengi.

 

Kanali Assimi Goita, kiongozi wa kijeshi wa Mali

 

Jeshi tawala nchini Mali lilisema katika taarifa iliyotangazwa Jumapili iliyopita kwamba serikali imeamua kujiondoa katika vyombo na idara zote za Kundi la G5, ikiwa ni pamoja na vikosi vya pamoja vya kupambana na makundi ya kigaidi. Kundi hilo lililoundwa mwaka wa 2014, lilizindua kikosi chake cha pamoja cha kukabiliana na ugaidi mwaka 2017.

Mali na baadhi ya nchi jirani zimekuwa kitovu cha makundi ya kigaidi. Ukosefu wa usalama katika eneo hilo unashuhudiwa katika hali ambayo Ufaransa imekuwepo kijeshi nchini Mali kwa miaka mingi, ikidai kuwa inapambana na ugaidi.