May 21, 2022 03:13 UTC
  • Faisal al-Miqdad: Kilichoiponza Syria na kuifanya iandamwe kwa vita ni himaya na uungaji mkono wake kwa Palestina

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria amesema kuwa, sababu ya nchi yake kuandamwa na vita ni hatua yake ya kuiunga mkono Palestina na kuwa pamoja na wananchi wa taifa hilo madhulumu.

Faisal al-Miqdad, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria amesisitiza kuwa, kilichoiponza nchi yake na kupelekea iandamwe kwa vita na makundi ya kigaidi yaliyokuwa yakipata himaya ya madola ya kigeni ni himaya na uungaji mkono wake kwa Palestina na Wapalestina.

Aidha amesisitiza kuwa, nchi yake itaendelea kuiunga mkono Palestina na harakati za ukombozi wa Palestina sambamba na kudumishha msimamo wake wa kupigania kukombolewa miinuko yake ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Aidha amesema, maeneo yanayokaliwa kwa mabavu yatarudi kwenye udhibiti wa serikali ya Syria; na wapiganaji wa Vikosi vya Kidemokrasia vya Wakurdi wa Syria wajue kwamba Wamarekani wavamizi wataondoka katika ardhi ya Syria na wao hawatakuwa na wa kumtegemea.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh nchini Syria

 

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria ameeleza kuwa, vipaumbele vya sera za nchi hiyo viko thabiti na akaongeza kuwa, wakati maadui wa Syria walipoona wameshindwa kuidhoofisha Syria ili kuilazimisha ibadilishe misimamo yake waliamua kutumia mbinu ya vita vya kigaidi dhidi yake.

Faisal al-Miqdad ameutaka Umoja wa Mataifa  na nchi za dunia kuyapitia matukio ya Syria kwa kina na kwa uadilifu na sambamba na kushirikiana na serikali ya Damascus, kuunga mkono pia jitihada inazofanya za kuinua na kuimarisha muelekeo chanya na athirifu wa kisiasa ili kuleta maelewano katika nchi hiyo ya Kiarabu.