May 21, 2022 07:54 UTC
  • Ugonjwa nadra wa monkeypox umeua watu 58 DRC

Kesi zaidi ya 1,300 za ugonjwa nadra wa monkeypox zimeripotiwa kote duniani na kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu hadi Mei nane watu 58 wamefriki dunia kutokana na ugonjwa huo ambukizi nchini Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani, mikoa 18 ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tayari ina kesi za virusi vya monkeypox.

Mwezi huu kesi kadhaa za kuenea kirusi cha monkeypox zimeripotiwa Ulaya na Amerika Kaskazini na walioambukizwa hawajapatikana kuwa na uhusiano wa kiepidemolojia na nchi za kati au magharibi mwa Afrika.

WHO inasema tokea Januari 1 hadi Septemba 13 2020 kulikuwa na kesi 4,584 za monkeypox na vifo 171 kutokana na ugonjwa huo nchini DRC.

Hadi kufikia Ijumaa nchi ambazo zilikuwa zimeripoti kesi za monkeypox ni pamoja na  Uingereza, Italia, Ureno, Uhispania, Uswidi, Ufaransa, Marekani, Canada na Australia. Monkeypox husababishwa na virusi vya monkeypox, kirusi cha familia moja ya virusi vya ndui, ingawa sio kali sana na wataalamu wanasema uwezekano wa kuambukizwa ni mdogo.

Inatokea zaidi katika sehemu za nchi za Afrika ya kati na magharibi, karibu na misitu ya kitropiki. Kesi ya kwanza ya ugonjwa huu iliripotiwa kwa mara ya kwanza huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika muongo wa 70 na kuenea kutoka mnyama hadi kwa mwanadamu baada ya kukaribiana.

Mikono ya mtu aliyeambukizwa monkeypox

Kuna aina mbili kuu za virusi - Afrika Magharibi na Afrika ya Kati. Dalili za awali ni pamoja na homa, kuumwa na kichwa, uvimbe, maumivu ya mgongo, kuumwa misuli na udhaifu wa mwili kwa ujumla.

Mara baada ya homa, upele unaweza kutokea, mara nyingi huanzia kwenye uso, kisha kuenea katika sehemu nyingine za mwili, kwa kawaida viganja vya mikono na nyayo za miguu. Upele, ambao unaweza kuwasha sana, hubadilika na kupitia hatua tofauti kabla hatimaye kutengeneza kipele, ambacho hutumbuka baadaye.

Moja ya njia za kuzuia maambukizi ni kupitia chanjo dhidi ya ndui ambayo imethibitishwa kuwa na ufanisi wa 85% katika kuzuia monkeypox. Tayari nchi za Ulaya na Amerika Kaskazini zimeshaanza kuagiza chanjo ya kukabiliana na monkeypox.

Taarifa zinasema Shirika la Afya Duniani, WHO, limeitisha kikao cha dharura kujali ugonjwa huu mpya.