May 21, 2022 12:29 UTC
  • Askari 11 wauawa katika shambulio dhidi ya kambi ya jeshi Burkina Faso

Wanajeshi 11 wa Burkina Faso wameuawa katika shambulio dhidi ya kambi ya jeshi iliyoko mkoani Kompienga mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na jeshi la Burkina Faso imeeleza kuwa, katika shambulio hilo dhidi ya kambi ya jeshi iliyoko kwenye mji wa Madjoari, mbali na askari 11 waliouawa, wanajeshi wengine 20 wamejeruhiwa na hivi sasa wanaendelea kupatiwa matibabu.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, jeshi  limefanikiwa kuwaua wanamgambo 15, ambao walikuwa wanajaribu kutoroka baada ya kutekeleza shambulizi hilo hapo jana.

Hadi sasa hakuna kundi lolote ambalo limekiri kuhusika na shambulizi hilo.

Shambulio hilo dhidi ya kambi ya jeshi limefanyika katika hali ambayo hivi karibuni jeshi la Burkina Faso liliwaua magaidi wapatao 50 katika operesheni mbili tofauti zilizotekelezwa kaskazini magharibi na kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba

Tangu mwaka wa 2015 Burkina Faso imekuwa ikipitia wakati mgumu kutokana na ongezeko la hujuma na mashambulio ya makundi ya kigaidi yanayoendeleza harakati zao katika maeneo ya kaskazini na magharibi nchini humo.

Mashambulio yanayofanywa na makundi hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu elfu mbili huku mamilioni ya wengine wakiyakimbia makazi yao kwa hofu ya kushambuliwa.

Jeshi la Burkina Faso lilimuondoa madarakani kiongozi wa kiraia Rais Roch Marc Christian Kabore mwezi Januari; na kiongozi wa jeshi aliyetwaa madaraka Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba amesema jukumu lake kubwa ni kumaliza makundi ya kigaidi na kurejesha usalama kwa raia.../