May 21, 2022 12:30 UTC
  • UN yataka Kenya, Somalia na Ethiopia zisaidiwe kukabili ukame

Umoja wa Mataifa umetoa mwito wa dharura wa kupatikana fedha ili kusaidia mataifa ya Pembe ya Afrika ambayo kwa miezi yameshuhudia hali ya ukame inayotishia kuwa mbaya zaidi.

Kwa mujibu wa Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeongoza Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura ya OCHA, muda wa kupoteza haupo tena na kwamba fedha hizo zinahitajika kwa haraka kuokoa maisha ya watu.

Umoja wa Mataifa umeeleza katika taarifa kuwa eneo la Pembe ya Afrika linashuhudia ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea, ambapo watu milioni 15 katika nchi za Ethiopia, Kenya na Somalia wanakabiliwa na baa la njaa.

Haya yanajiri wakati huu viongozi wa nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakiwataka raia kujiwekea akiba ya kutosha ya chakula.

Mwishoni mwa mwaka jana, Umoja wa Mataifa ulizindua kampeni ya kukusanya dola za Marekani bilioni 41 kusaidia watu milioni 274 wanaohitaji msaada na ulinzi.

Kabla ya wito huo, ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura OCHA, ilishatahadharisha pia kwamba, watu wapatao milioni 18 kwenye Ukanda wa Sahel barani Afrika watakumbwa na njaa kali na kutokuwa na uhakika wa chakula katika kipindi cha miezi mitatu ijayo ikiwa ni idadi kubwa zaidi tangu mwaka 2014.

Duru mbalimbali za habari zinasema, watu wengi wamekuwa wakikabiliwa na njaa tangu mwaka 2014 wengi wao wakitokea Burkina Faso, Chad, Mali na Niger wakati milioni 1.7 miongoni mwao wakihitaji misaada ya dharura ya chakula.

Hali hiyo inasemekana kuwa inatokana na athari za vita vya Russia nchini Ukraine, janga la corona, mabadiliko ya tabianchi pamoja na kupanda kwa gharama ya maisha.../

 

Tags